Halmashauri ya Wilaya ya Maswa chini ya usimamizi wa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji imefanya sherehe za kuwapongeza Walimu wote wa shule za Msingi Wilayani hapa kutokana na ufaulu mzuri walioupata mwaka huu 2019. Sherehe imehudhuliwa na wadau mbalimbali wa elimu ikiwa ni pamoja na Katibu wa CWT Taifa ambaye alikuwa Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Kamati ya Siasa Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Maswa, Wenyeviti wa CWT mikoa ya Mara, Shinyanga, Kigoma na Simiyu, Madiwani wa Halamashauri ya Wilaya ya Maswa, Mbunge wa Maswa Mashariki na Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Muwakilishi wa Mbunge wa Maswa Magharibi, Wadau mbalimbali wa Elimu Wilayani Maswa, Wakuu wa Idara na Vitengo Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Walimu wote Wilayani Maswa, Wakuu wa Wilaya Mkoa wa Simiyu na Wakurugenzi Watendaji Wilaya / Mji wa Mkoa wa Simiyu.
Katika sherehe hii matukio mbalimbali yamefanyika ikiwemo na;
Kukabidhi kiwanja kwa Chama cha Walimu kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha Mikate inayotokana na unga wa viazi lishe.
Imefanyika harambee ya kuchangia ujenzi wa Nyumba za walimu na ukamilishaji wa nyumba za walimu ambazo zmeshaanza kujengwa huko katika shule za Jihu, Busamuda, Jilago na Buhangija ambapo Pesa kiasi cha Tsh. 32,700,000/= kimepatikana na Saruji mifuko 265 imepatikana.
Umefanyika uzinduzi wa mfuko wa kusaidia Walimu ambapo kwa kuanza kiasi cha Tsh.30,000,000/= kimepatikana kwa ajili ya kutunisha mfuko huo ili walimu waweze kukopeshwa kwa riba nafuu na kuepuka kugawa kadi zao za benki kwa wakopeshaji wadogo wadogo. Mfuko umezinduliwa rasmi na wadau wafuatao wametunisha mfuko kwa kuchangia kiasi cha fedha; Chama cha Walimu Tanzania CWT wamechangia Tsh. 8,000,000/=, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Tsh. 15,000,000/= na Mhe. Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki Tsh. 6,000,000/=.
Mgeni rasmi amekabidhi zawadi kwa shule 5 zilizofanya vizuri sana ikiwa ni cheti na pesa taslimu tsh.500,000/= kwa kila shule na amekabidhi majiko ya gesi kwa shule zote za Msingi ikiwa ni ishara ya kuzindua unywaji wa Chai kwa walimu ndani ya mazingira ya shule.
Akihutubia hadhara hiyo Mgeni rasmi amewaasa walimu kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka ikiwa ni sambamba na kutunza nidhamu na maadili ya ualimu. Amesema matatizo yote ya walimu yanajulikana hivyo basi mazungumzo na serikali yanaendelea ili yote yaweze kutatulika ikiwa ni pamoja na waraka ambao ulitoka na kuwataka walimu wote wanaotoka masomoni wasipande madaraja yao wanayostahili.
Pamoja na changamoto hizo hakuwa nyuma kuishukuru Serikali kwa hatua inayochukua pale changamoto zinapojitokeza ikiwa ni pamoja na kupandisha madaraja na kulipa malimbikizo ya walimu hasa malimbikizo ya mishahara.
Amesema wapo watumishi wengi ambao hawakupanda madaraja kutokana na kutokuwepo kwenye mpango, tatizo hili linatatuliwa kwa ushirikishwaji wa chama cha walimu na ofisi ya utumishi kwa kutengeneza mpango kazi. Amesisitiza sana Walimu kujiunga na benki ya Mwalimu ili waweze kukopesheka kiurahisi kupitia mfuko uliozinduliwa.
Aidha ameshukuru sana kwa ushirikiano wa viongozi mbalimbali wa Mkoa na Wilaya kwa Walimu hasa kwa kubuni jambo jema litakalo inua uwajibikaji kwa walimu kwani sherehe hii ni ya mfano Tanzania.
Sambamba na hayo CWT imetoa Tsh.10,000,000/= kwa ajiri ya usafiri kuwarudisha shuleni kwao walimu wote waliohudhulia sherehe hii.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.