Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imekabidhi mkopo wa shilingi milioni 173.6 kwa vikundi 15 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa awamu ya kwanza ikiwa ni sehemu ya asilimia kumi ya mapato yake ya ndani katika mwaka wa fedha unaoendelea.
Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bi. Basila Bruno wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika ukumbi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa tarehe 26 Machi 2025.
Amesema katika awamu ya kwanza ya mkopo huo vikundi vya wanawake 7 vimekopeshwa shilingi milioni 78.9, vikundi vya vijana 5 vimepokea milioni 81, pamoja watu wenye ulemavu vikundi 3 vimekopeshwa milioni 13.7.
Pia Bi. Bruno ameongeza kuwa Halmashauri imeweza kutenga na kutoa mikopo kwa makundi yote ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuongeza kipato kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutokana na miradi yao na hivyo kuchangia pato la Halmashauri ya Wilaya na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bw. Robert Urassa amewataka wanufaika wote wa mikopo kuhakikisha fedha hizo wanazozipata zikafanye shughuli inayotakiwa na kuweza kuzilejesha kwa wakati.
“Wanaohitaji mikopo hii ni wengi na nyie mmebahatika kupata mikopo hii kwa awamu ya kwanza tunahitaji mkafanye kile mlichotarajia kukifanya ili mrejeshe fedha hizi kwa wakati ili wanawake wengine, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri yetu ya Maswa waendeleee kunufaika.”amesema Bw. urassa
Pia ametoa wito kwa vikundi hivyo kuhakikisha vinatakeleza malengo yaliyokusudiwa katika biashara kwa kuwa Halmashauri imewapa mitaji ili waweze kujiendesha na amesisistiza kuwa zoezi hilo ni endelevu ambapo awamu ya pili ya utoaji wa mikopo itaendelea katika vikundi vingine vilivyoomba.
Akikabidhi hundi kwa vikundi, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mh. Vincent Anney amesema fedha hizo sio fedha za kunywea pombe, kununua shamba mikopo hiyo ni kwa ajili ya kwenda kuanzisha biashara ndogondogo ambazo zitakwenda kuwapa mtaji ili baadae wajitegemee.
“Naomba sana tumsaidie Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa yeye mwenyewe aliamua kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo ya asilimia kumi kwa nchi nzima kwa kutunga sheria na kubadilisha utaratibu, Dkt Samia anataka watanzania wajikomboe ili wajikomboe fedha hii ya mikopo lazima ilejeshwe na ili irejeshwe unatakiwa uishi kwenye mpango kazi wako wa biashara.” ameeleza Dkt Anney
Pia ametoa wito kwa vikundi vyote kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati bila kuongeza muda kwa kuweka mpango kazi wa kulipa mkopo huo ili watu wengine waweze kupata fursa ya kukopeshwa mikopo hiyo.
Aidha amewapongeza wanawake wote kwa kuwa mstari wa mbele kulipa mikopo na kuwataka vijana kuepuka tabia za kutokulipa mikopo hiyo kwa wakati.
Pia amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji kuwasilisha majina ya vikundi vyote vinavyodaiwa katika ofisi ya TAKUKURU ili watu hao wafikishwe mahakamani ili fedha hiyo iweze kurejeshwa.
Kwa upande wa vikundi vilivyonufaika na mikopo hiyo vimeishukuru serikali ya awamu ya sita ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo hiyo kwa kuwa sasa itawasaidia kufanya shughuli ambazo wamekusudia na kuahidi kurejesha kwa wakati mikopo hiyo ili na wengine wapate mikopo hiyo.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.