Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuboresha sekta ya ardhi kwa kuandaa mpango wa matumizi sahihi ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa yenye lengo la upangaji unaoainisha matumizi sahihi ya rasilimali ardhi kulingana na mahitaji ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Hayo yameelezwa na Afisa Mipango Miji Mkuu kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ndg. Aristides Mulokozi wakati akitambulisha mradi huo kwa Madiwani, kamati ya ulinzi na usalama, wataalamu wa Halmashauri na Watendaji wa Kata katika kikao cha baraza la madiwani lililofanyika leo tarehe 2 March 2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Ndg. Mulokozi amesema Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ni miongoni mwa Halmashauri sita zilizopata fursa ya kupitiwa na mradi huo kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu, kukua kwa sekta za miundombinu pamoja huduma za kiuchumi na kijamii.
Mpango huo upo kisheria kwa ajili ya kutatua changamoto kwa kuzuia uharibifu wa ardhi na rasilimali zake, kulinda maeneo ya uwekezaji na kuratibu mipango ya maendeleo ya kisekta inayohusiana na upangaji wa matumizi ya ardhi na hivyo kupelekea matumizi endelevu ya rasilimali za ardhi katika Wilaya.
Aidha, ndg. Mulokozi amesema kuwa mpango huo hautajikita katika mambo ya ardhi peke yake utajumuisha maeneo mengine kwa sababu mradi huo utapita kila Kata kuchukua taarifa za kidemografia na kijamii, pamoja na uboreshaji wa Ofisi za ardhi za Wilaya na za vijiji pamoja na kutoa hati za kimila.
Ameongeza kuwa mradi huo utadumu kwa muda wa miaka 20 hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi kutokana na mipango ya Halmashauri ya Wilaya kuainisha miradi ya maendeleo inayopaswa kutekelezwa na pia itasaidia kutatua migogoro ya ardhi.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ndg. Simon Berege ameishukuru Wizara ya Ardhi, Nyumba, na maendeleo ya makazi kwa kuleta mradi huo ambao utaleta mabadiliko makubwa katika Wilaya ya Maswa na kutatua matatizo ya kijamii na migogoro mbalimbali.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.