Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Simon Berege ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi Cha shilingi bilioni 7,155,691,986/= kutoka serikali kuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akisoma taarifa katika kikao Cha Baraza la madiwani Cha robo ya tatu kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg Berege amesema katika robo ya tatu serikali imetoa Fedha kwa asilimia mia moja katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa na tayari miradi hiyo inaendelea mingine inaanza ikiwepo ujenzi wa matundu ya vyoo 41 katika shule sita, ujenzi wa shule tatu mpya, ununuzi wa vifaa tiba na mingine mingi inatekelezwa katika sekta za Elimu na afya.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita imetoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la Halmashauri ambalo litajengwa Kata ya Nyalikungu katika kitongoji cha Ng'hami
Ndg Berege ameeleza kuwa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameipatia Fedha Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa ajili ya ujenzi wa VETA mpya kubwa na ya kisasa ambayo itajengwa katika Kata ya Sola karibu na Shule ya msingi Sola na itasimamiwa na chuo Cha maendeleo ya wananchi Malampaka.
Aidha amesisitiza kuwa wataalamu tayari walifika eneo la mradi na kuridhishwa na eneo hilo ambapo amesema matangazo tayari yameshatoka ili wazabuni wapatikane pamoja na wajenzi ili ujenzi uanze.
"Sisi watendaji na madiwani wote tutatoa ushirikiano, itakuwa ni suluhisho kubwa kwa vijana wetu kwa sababu mradi mkubwa sana na utaleta mabadiliko makubwa sana katika Halmashauri yetu" amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Nao madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wamempongeza Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuleta Fedha za miradi ya maendeleo na wameahidi kumuunga mkono kwa kusimamia miradi mbalimbali katika kata zao.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa wilaya ya Maswa Ndg Agness R Alex akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge katika salamu za serikali amesema msimu wa pamba umefunguliwa hivyo amewataka wanunuzi kufuata Sheria na taratibu za ununuzi wa pamba na amewataka wananchi wa Maswa kuhakikisha pamba yote inanunuliwa katika maeneo yaliyotegwa kwa ajili ya kuuzia pamba, na yeyote atakayetorosha pamba kwenda nje ya Maswa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Pia ametoa wito kwa madiwani pamoja na wataalamu wa Halmashauri kusimamia miradi ili ikamilike kwa wakati na kujali thamani ya Fedha.
" Kila Mhe Diwani kwenye eneo lake ahakikishe miradi iliyopo kule inakamirika na kutekelezwa kwa wakati, yale ambayo wananchi wanatakiwa kuyafanya wayafanye tuwahamasishe wananchi wafanye, na yale ambayo sisi serikali tunatakiwa kufanya tuyafanye, sisi kama watendaji tunatakiwa tuyafanye kwa wakati na mwisho wa siku thamani ya Fedha inaonekana na mradi unaonekana" amesema Katibu Tawala.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.