Mwenyekiti wa UWT Taifa Ndg. Mary Chatanda amempogeza Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa Fedha nyingi hususani katika ujenzi wa shule za Msingi na Sekondari pamoja na miundombinu mingine ambayo inatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
"Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa Fedha nyingi ili watoto wetu waweze kusoma, jukumu letu sisi wazazi ni kushirikiana na serikali kuhakikisha kwamba mnawaandaa watoto waweze kwenda shule sio serikali ijenge majengo halafu baadhi ya watoto hawaendi shule, watoto wote wenye umri wa kwenda shule kuanzia hawa wadogo wa kwenda shule kuanzia hawa wa chekechea pale wamejengewa shule nzuri sana ya chekechea wapelekeni watoto shule". Amesema Ndg Chatanda.
Amezungumza hayo kwa nyakati tofauti wakati akikagua na kuongea na wananchi katika maeneo mbalimbali ya miradi ya maendeleo aliyoitembelea leo tarehe 17.09.2023 katika Wilaya ya Maswa na kuridhishwa na miradi hiyo ambayo imetekelezwa kwa ufanisi.
Aidha Mwenyekiti wa UWT Taifa ametoa wito kwa jamii kuwapeleka watoto wa kike shule na kuachana na Mila potofu za kuwaozesha pindi tu wanapofika hatua ya kubalehe hivyo amewasisitiza wazazi kuwa urithi wa mtoto wa kike ni kufika chuo kikuu na hata kama atashindwa kufaulu darasa la saba au kidato cha nne au sita serikali kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi inajenga vyuo vya VETA kila Wilaya lengo ni kuwasaidia vijana na mabinti kupata Elimu ya ufundi ambayo itawasaidia kupata maarifa ya kujitegemea na kuacha kuwa tegemezi.
Pia Ndg Chatanda amewaomba wazazi kuwasimamia vizuri watoto kwa kuwa kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa watoto hivyo amewasihi wazazi kukaa na watoto wao kwa kuwaelekeza na kuwalea watoto katika maadili mema na ameiomba jamii kuwafichua watu wote wanaowafanyia ukatili watoto hasahasa wanafunzi ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya Dora.
Pia amewataka wananchi wote kupima afya zao katika vituo vya kutolea huduma ya afya wakiwepo akina mama wajawazito ili kuepuka matatizo ya vifo vya uzazi vinavyoweza kutokea pindi ambapo mama amejifungulia nyumbani.
Ameongeza kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kupitia mama Samia Suluhu Hassan imeandaa utaratibu mzuri kwa ajili ya mikopo ya asilimia kumi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu nia ya serikali ni kuwaondoa wanawake katika mikopo ya kausha damu na mwendo kasi kwa kuwa mikopo ya serikali haitakuwa na riba na itakopeshwa kupitia benki ya NMB na CRDB na itatolewa kwa mtu mmoja mmoja atakayetaka kukopa.
Akiwa Wilayani Maswa Ndg Chatanda ametembelea miradi mbalimbali ambapo ametembelea na kukagua Shule mpya ya Majengo iliyopo katika Kata ya Shishiyu ambayo ujenzi wake upo katika hatua ya ukamilishaji ambapo kiasi cha shilingi milioni 348,500,000/= kimetolewa na serikali kupitia mradi wa BOOST, amekagua ujenzi wa Kituo cha afya kilichopo Kata ya Shishiyu chenye thamani ya Shilingi milioni 500,000,000/=, Zahanati ya Barikiwa, Jengo la dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa ambalo lilipata Fedha kiasi cha shilingi milioni 300,000,000/= kutoka serikalini kupitia Fedha za Uviko19 lengo likiwa ni kuboresha huduma zote za matibabu ikiwepo ya dharura.
Pia ametembelea shule kongwe ya Shanwa ambayo ilianzishwa mwaka 1928 na kuona ukarabati uliofanyika ambapo shilingi milioni 100,000,000/= zilitolewa na serikali kuu kwa ajili kukarabati vyumba vya madarasa 10 na ofisi 4 lengo likiwa ni kuboresha Mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi pamoja na kutembelea na kukagua kiwanda cha Sola ambacho kinajishughulisha na uchakataji wa zao la Pamba ambapo serikali ilikifufua kiwanda hicho kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 5 kutoka benki ya maendeleo TDB ambapo kinafanya kazi mpaka sasa .
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.