Watendaji wa Kata na waganga wa tiba asilia wamepata elimu ya matumizi ya vifaa maluum vya kuwapima watoto katika maeneo yao na kuwapa uelewa watendaji wa Kata wanapopewa taarifa na watendaji wa vijiji waweze kubaini watoto wenye udumavu, ukondefu pamoja na uzito pungufu ili wapelekwe hospitali kwa ajili ya matibabu.
Pia amesema waganga wa tiba asilia na watendaji wa Kata wanatakiwa kuwa na vifaa hivyo ili kabla ya kumtibu mgonjwa aweze kujua yupo katika hali gani, pia kifaa hicho kina uwezo wa kubaini hali ya mtoto ya lishe kwa kuangalia rangi ambazo zinaonyesha katika kifaa hicho ambapo ikiwa nyekundu huyo mtoto anakuwa katika hali ya hatari na ikiwa njano anakuwa salama.
Hayo yamesemwa na Afisa lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Abel Gyunda wakati akitoa semina hiyo katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Afisa lishe amesema waganga wa tiba asili wanasaidia lakini tatizo la lishe haliwezi kutatuliwa na Mganga wa tiba asili ndio maana wameshirikishwa katika kikao hicho ili kupata elimu ya kuwatambua watoto wenye dalili za utapiamlo mkali na kutoa taarifa kwa mhudumu wa afya au mganga mfawidhi katika kituo kilicho karibu yake.
Ndg. Gyunda ameongeza kuwa katika Mkoa wa Simiyu kufikia mwaka jana takwimu za hali ya udumavu ilikuwa 32.1% ambapo katika watoto 100 watoto 32 wamepata udumavu, uzito pungufu ulikuwa 14.6% na ukondefu ulikuwa kwa 4.6% hiyo yote ni kwa sababu ya kutokupata lishe sahihi.
Afisa lishe amesema tatizo la lishe Duniani ni kubwa ili kukabiliana na tatizo hilo viongozi wana wajibu wa kuwaelimisha akina mama kutumia virutubisho vyenye madini chumvi, vitamin A na dawa za minyoo lengo la kurutubisha chakula ni kuondokana na matatizo makubwa ambayo yanasababishwa na ulaji wa vyakula duni hivyo vyakula vikirutubishwa vitasaidia akina mama kuepuka kujifungua watoto wenye matatizo kama kuvimba kichwa.
Aidha, Ndg. Gyunda amewasisitiza watendaji wa Kata na waganga wa tiba asili endapo watambaini mtoto mwenye dalili za udumavu, ukondefu wanatakiwa kutoa taarifa kwa wahudumu wa afya ili mtoto huyo aanzishiwe matibabu mara moja kwa kuwa tayari wamepewa vifaa maalumu ambavyo vitawasaidia kutambua mtoto kama ana dalili zozote za ugonjwa huo.
Afisa lishe ameendelea kusema katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kupitia mapato ya ndani imetenga bajeti zaidi ya shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuwaelimisha waganga wa tiba asili, watendaji wa vijiji, watendaji wa kata na wahudumu wa afya katika masuala ya afua za lishe ili tatizo la utapiamlo kwa Wilaya ya Maswa liwe historia.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.