Mratibu wa sensa ya watu na makazi wilaya ya Maswa mkoani Simiyu Ndg Ntobi Ntambi leo ameanza ziara katika Kata mbalimbali za wilayani Maswa ambazo ni Budekwa, Mwabaraturu na Busilili, yenye lengo la kutoa elimu kwa kamati tatu za sensa ambazo zitakuwa na majukumu ya kuhamasisha wananchi kuhusiana na zoezi hilo la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Augusti 23, 2022.
Akitoa elimu hiyo mratibu amesema zoezi hilo litakuwa na utofauti na mazoezi mengine yaliyopita kwa sababu muundo unaotumika mwaka huu utakuwa na kamati tatu ambazo ni Kamati ya Kitongoji, Kamati ya Kijiji na Kamati ya Kata. Hivyo amewaomba wanakamati kuzingatia majukumu yao kama ambavyo yameainishwa kwenye muongozo.
Kutokana na umuhimu wa zoezi hilo Ndg Ntobi amewasisitiza wanakamati hao kutumia mbinu za ziada ikiwepo vikundi vya wasanii "Manju" wanaopatikana maeneo yao ili waweze kutunga nyimbo zinazohusu sensa, vikao, mikusanyiko mbalimbali na mikutano ili ujumbe uwafikie wananchi wengi kwa muda mfupi.
Kwa upande wao wanakamati hao kwa nyakati tofauti wameipongeza Serikali na kuahidi kuwa watakuwa makini katika zoezi hilo na watatoa ushirikiano kuhakikisha zoezi hilo linaanza vizuri na kukamilika kwa ufasaha kwa kuwa dozi wameipata na wataitendea haki katika kuhamasisha wananchi wao.
Mratibu amewaomba wanakamati kuanzia kesho zoezi hilo litekelezwe kwa Kamati hizo zote kuanzia ngazi ya Kitongoji mpaka ngazi ya Kata na kauli mbiu ya sensa mwaka huu ni "Sensa kwa maendeleo jiandae kuhesabiwa"
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.