Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Maswa imekagua mradi wa kisima chenye urefu wa mita 120 chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 19,000 kwa saa sawa na lita 456,000 kwa siku ambapo ujenzi wa kisima hicho ukikamilika utaweza kuhudumia wananchi 8361 wa Kijiji cha Ipililo Kata ya Ipililo.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama Wilaya ya Maswa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge amesema Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anataka wananchi wake wawe na furaha ikiwemo usalama, utulivu na amani pamoja na utoaji wa huduma za kijamii na za kiuchumi kwa wananchi.
Mhe Kaminyoge amesema hayo katika mkutano wa hadhara alioufanya katika Kijiji cha Ipililo wakati akizungumza na wananchi hao baada ya kamati ya usalama ya wilaya kuhitimisha ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Mhe Rais alisikiliza maombi ya wananchi kupitia kwa viongozi mliowachagua mheshimiwa Diwani, Mhe Mbunge ambaye ni mwakilishi wa wananchi kupeleka malalamiko yenu kwa Mhe Rais, Mhe Rais amesikia na ametoa kiasi cha shilingi bilioni 1.3 katika Kijiji cha Ipililo kwa ajili ya huduma ya maji.” amesema Mhe Kaminyoge
Pia amesema tayari kisima kirefu kimechimbwa na mkandarasi tayari yupo “site” akijenga jengo la miundombinu ya kuingiza umeme, pampu ili maji yaweze kuvutwa na kupelekwa kwenye tenki kwa ajili ya kupokea maji kutoka kwenye kisima ili kusambaza maji hayo sehemu mbalimbali za wananchi.
Mhe Mkuu wa Wilaya ameeleza kuwa mkataba wa mkandarasi ni wa mwaka mmoja hivyo amemuomba kuharakisha mradi huo kwa kuwa mkandarasi huyo anafanya kazi kwa weredi mkubwa kwa kuwa tatizo la ukosefu wa maji kwa wananchi wa Ipililo ni kubwa na mkandarasi huyo ameahidi kufikia mwezi wa Tano mwaka huu wananchi watapata maji.
Ujenzi wa mradi huo unatekelezwa na wakala wa maji na Usafi wa Mazingira vijijini RUWASA.
Pia katika hatua nyingine Mhe Kaminyoge amesema Mhe Rais ametoa kiasi cha shilingi milioni 79 kwa Kijiji cha Ikungulyankoma na Kijiji cha Ipililo shs milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana wanaotoka mbali ili waweze kukaa shuleni na kuepukana na mimba zisizotarajiwa.
Amesema mradi huo unatekelezwa kupitia miradi ya TASAF yenye masharti ya wananchi kuchangia nguvu kazi katika ujenzi huo ambapo tayari awamu ya kwanza ya ujenzi wa bweni imefanyika katika shule ya Sekondari Budekwa na sasa mradi huo utafanyika katika shule ya Sekondari Ipililo hivyo amewataka wananchi kuchangia nguvu kazi ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.
Akizungumza kwa nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ametoa siku tatu kwa mkandarasi kuhakikisha anatengeneza Barabara zote ambazo ni korofi ili ziweze kupitika wananchi waweze kusafirisha mazao yao, ambapo Barabara hizo ni Barabara ya Njiapanda- Muhida yenye gharama ya shs milioni 57 kutoka mfuko wa barabara.
Matengenezo ya Daraja la Wigelekelo Barabara ya Mwasayi- Masela yenye gharama ya Tsh milioni 325 ambapo mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 75%, mradi wa Barabara ya Bushashi – Ipililo wenye gharama ya Shs milioni 400 fedha hizo zimetoka mfuko wa tozo za mafuta.
"Sisi tunaopewa hela na serikali kwa ajili ya kutengeneza miundombinu na huduma mbalimbali za wananchi tusiwe kikwazo kwa wao kupata huduma nzuri, hizi Barabara sio za TARURA ni za wananchi wa Maswa kwa usimamizi wa Mkuu wa Wilaya." Amesema mkuu wa wilaya.
Pia amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa makalavati yote kwa muda wa wiki moja katika Barabara hizo.
Pia kamati ya usalama ya Wilaya imekagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Maswa lililopo Ng'hami Kata ya Nyalikungu pamoja na ujenzi wa tanki la maji Mwashegeshi mradi unaosimamiwa na MAUWASA.
Jengo la Utawala la Halmshauri
Tank la Maji Mwashegeshi
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.