Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wamepata elimu ya mfumo wa stakabadhi ghalani yenye lengo la kuwajengea uwezo Madiwani na wataalamu kuhusu matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwaelimisha wakulima katika kuuza mazao ili wakulima wawe na uhakika wa kuuza mazao kwa bei wanayoitaka.
Hayo yamesemwa na Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoa wa Simiyu Bw. Godfrey Mpepo katika kikao cha Baraza la madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2023/2024 kilichofanyika tarehe 16.11.2023 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambapo madiwani walikuwa wakiwasilisha taarifa za Kata zao.
Alisema. Mfumo wa stakabadhi ghalani ni hati iliyopo kwenye karatasi au mfumo wa mtandao ambayo inatolewa kwa mwenye mali ambaye ni mkulima baada ya kupeleka mazao yake kwenye ghala husika ambalo linakuwa limepewa leseni na Mamlaka ya maghala nchini.
"Mfumo wa stakabadhi ghalani unahamasisha sana na unakusudia sana kupokea mazao ghalani yale yenye ubora, na huo ubora unathibitishwa kwa vipimo kila zao linapimwa kwa vifaa vyake hata likipelekwa nje ya nchi linaitangaza Tanzania aidha hizi dengu, choroko au pamba zimetoka Tanzania zikiwa na ubora wa kimataifa." Amesema Mpepo
Aidha Mpepo amesema dhumuni kubwa la stakabadhi ghalani ni kurasimisha mifumo ya masoko kwa lengo la kupinga vipingamizi mbalimbali vinavyosabanisha kukwamisha uzalishaji wenye tija na utafutaji wa masoko wa mazao yanayozalishwa.
"Uzuri wa stakabadhi ghalani unapata mazao yenye ubora kabisa kwa maana kwamba mazao yanakuwa bora ili yaweze kuingia sokoni ni lazima yathibitishwe na vipimo vya ubora wa soko au wa zao husika kwa maana kwamba mazao mengi nchini kwetu yanakuwa yamenunuliwa kwenda kutumiwa nje ya nchi ili yaweze kwenda nje kimataifa yanatakiwa kuthibitishwa". Amesema Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika
Kaimu Mrajisi wa vyama vyaushirika amesema taarifa za mkulima zikiwepo mtandaoni zitamsaidia katika masoko kuongeza bei katika mazao pamoja na kuondoa uhaba wa mitaji kwa sababu mkulima akizalisha taarifa zake zitapatikana mtandaoni hivyo kumfanya aweze kupata mkopo benki.
Mfumo huo pia utasaidia wanunuzi wengi kununua mazao mbalimbali ambayo yataliongezea Taifa Fedha za kigeni ambazo zitachangia kuongeza mapato kwa upande wa serikali kutokana na wanunuzi kutoka nchi mbalimbali wataweza kununua mazao hayo kwa njia ya mtandao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mpindo Mhe. Amos Ntambo amewashukuru wataalamu kwa kuja na wazo hilo la kuanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kuwa ni mfumo mzuri ambao utawasaidia wakulima kupata bei nzuri na kuzisaidia Halmashauri za Mkoa wa Simiyu kuongeza mapato na pia madiwani wameomba elimu itolewe zaidi ili wawe na uelewa zaidi.
Stakabadhi ghalani inahusisha masoko level ya mtandao yaani unaweza ukauza bidhaa kupitia mtandao, na tayari Mikoa ya Mtwara, lindi na Songwe wanatumia mfumo huo wa stakabadhi ghalani ambao umewasaidia wakulima kupanga bei za mazao katika soko kwa sababu taarifa zote za bei zinakuwa mtandaoni.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.