Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wamepata mafunzo ya matumizi ya vishikwambi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo katika Kata zao ikiwemo taarifa za kata ambazo zitasomwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023.
Akitoa semina hiyo katika ukumbi Mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Afisa TEHAMA Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Edwin Bairu amewasisitiza waheshimiwa Madiwani kuwa, Baraza na Kamati zote zitatumia teknolojia ya kidigitali katika kuendesha shughuli zote za vikao kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa tayari imenunua vishikwambi vitakavyotumika kwa matumizi ya vikao hivyo ambavyo tayari vimewekewa programu maalumu ambayo taarifa zote zitatumwa humo.
Aidha Afisa TEHAMA amewasihi waheshimiwa Madiwani kutumia wenyewe vishikwambi na si vinginevyo ili kuepusha uharibifu utakaojitokeza ikiwepo kuvunjika au kupotea na kuweka taarifa katika usalama. Pia amewaomba waheshimiwa Madiwani kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili wapate uzoefu haraka wa kutumia vishikwambi hivyo.
Akizungumza katika semina hiyo Afisa manunuzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa amewasihi waheshimiwa Madiwani kuvitunza vishikwambi hivyo kwa kuwa ni Mali ya serikali pamoja na kuvitumia kwa matumizi ya serikali tu na si vinginevyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa amewaomba waheshimiwa Madiwani kufanya kazi kwa karibu na watendaji wa Kata zao katika kuandaa taarifa zao na usimamiaji wa miradi maendeleo. Pia amewasisitiza waheshimiwa Madiwani ambao hawajapata vishikwambi wawe na subira kwa kuwa bajeti iliyowekwa imetosha vishikwambi vya Madiwani wa kata 36 tu ambavyo vitasaidia utendaji kazi wa waheshimiwa Madiwani na kupunguza gharama za uendeshaji wa vikao na kuongeza ufanisi.
Kwa upande wao waheshimiwa Madiwani wamefurahi kupata elimu hiyo na kuiomba Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuona utaratibu wa kufanya ili Madiwani wa viti maalum nao waweze kupata fursa ya kupata vishikwambi ili kuleta chachu ya uwajibikaji.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.