Maafisa Ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu wamepata mafunzo ya kanuni bora za kilimo cha zao la Karanga yenye lengo la kuwajengea uwezo wa namna ya kukabiliana na magonjwa mbalimbali, nafasi ya upandaji na matumizi ya mbegu bora za Karanga.
Mafunzo hayo yametolewa na wataalamu kutoka Taasisi ya Kilimo Tanzania TARI leo tarehe 6.11.2023 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambapo maafisa ugani zaidi ya 20 wamehudhuria kwa ajili ya kupata mafunzo hayo ili wakawawezeshe wakulima kulima kilimo bora ambacho kitawasaidia kuvuna mavuno kwa tija.
Akitoa elimu hiyo mratibu wa program ya utafiti wa zao la Karanga nchini Dr Happy Daudi kutoka kituo cha Naliendele amesema wamefika katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa kwa ajili ya kuwajengea uwezo maafisa ugani wote kuhusu kilimo bora cha zao la Karanga kwa kuwa wao ndio wanaoweza kutatua changamoto mbalimbali za wakulima.
Ameongeza kuwa katika kilimo cha Karanga wakulima wengi hawatumii mbegu bora za Karanga hivyo kupitia mafunzo hayo Dr Happy ametoa wito kwa maafisa ugani kuanzisha vikundi vya kuzalisha Karanga ili kupata mbegu bora ambazo zimethibitishwa kitaalamu na taasisi za utafiti wa kilimo.
Pia amesema kutokana na mafanikio waliyoyapata wakulima ambao walilima mbegu aina ya Mangaka 2009 taasisi hiyo imetoa kilo 100 za mbegu hiyo ya Mangaka 2009 kwa kuwa ni mbegu nzuri inayofaa kwa ardhi ya Maswa ambapo katika eneo la nusu heka wakulima wamepata gunia 16, ili kutanua kilimo chao maafisa ugani wana jukumu la kuwajengea uwezo wakulima kutumia mbegu bora na kufuata kanuni za kilimo bora cha Karanga.
Nae Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Masalu Shibiliti ameishukuru taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele kwa kutoa mafunzo hayo kwa Maafisa Ugani ambayo yatawasaidia wakulima kulima kilimo ambacho kitazingatia mbegu bora kwa kuwa wakulima wengi wa Wilaya ya Maswa hawatumii mbegu bora za Karanga hivyo ujio wa mbegu hizo utaongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.
Ameongeza kuwa wakulima wa Maswa watanufaika kutokana na elimu hiyo kwa kuwa maafisa ugani wataweza kuwaelimisha namna ya kupanda kwa kuzingatia kanuni za upandaji wa sentimeta 10 kati ya mmea na sentimeta 50 kati ya mstari, udhibiti wa sumu kuvu na magonjwa mbalimbali katika zao hilo lengo likiwa ni kumfanya mkulima kupata matokeo.
Aidha mafunzo hayo yatawasaidia maafisa ugani kuwaelimisha wananchi kutumia mbegu bora za zao la Karanga sambambamba na hilo Halmashauri itaunga mkono jitihada hizo kwa kuweka kipaumbele cha zao hilo katika maonyesho ya wakulima nanenane ili wakulima wengi wapate elimu hiyo na kuanzisha mashamba darasa kila Kata ambapo mpaka sasa tayari Kata 3 zimeanza uzalishaji.
Kwa upande wake Afisa Ugani wa Kata ya Isanga Fred Fidelis amesema katika Kata yake wakulima walikuwa wanalima mbegu zisizo za kisasa hivyo kupitia mafunzo hayo wanaishukuru taasisi hiyo ya Naliendele kwa kuwapatia mbegu za kisasa ambazo zitawasaidia wakulima.
Nae Bibi shamba wa Kata ya Nyalikungu Elin Nashoni amewashukuru wataalamu kwa mafunzo hayo ambayo yamekuja kwa muda sahihi ambapo wakulima watapata elimu ya namna bora ya kulima kwa nafasi ya upandaji wa mbegu hizo hivyo kupitia wataalamu tayari Wilaya ya Maswa imeanzisha vikundi ambavyo vitazalisha mbegu ambazo baada ya miaka miwili Maswa itapata mbegu bora za karanga ambazo zitatumika kwa ajili ya uzalishaji.
Godson Makoye Afisa kilimo Kata ya Sukuma anaishukuru serikali kupitia taasisi ya utafiti wa kilimo TARI Naliendele kwa mafunzo waliyoyatoa ambayo yamewasaidia kujua aina mbalimbali za Karanga na kulima bila kuchanganya na zao lingine hivyo ameahidi kupitia mafunzo hayo atawaelekeza wakulima kupitia mashamba darasa kulima kwa tija ili wapate magunia 20 na kuendelea kwa heka tofauti na sasa ambapo wanapata magunia 2 mpaka 3.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.