Maadhimisho ya miaka 61 ya uhuru yamefanyika wilayani Maswa kwa kongamano lililohusisha wadau mbalimbali kujadili maendeleo endelevu yaliyofanyika wilaya ya Maswa kwa kuangazia sekta mbalimbali za wilaya ya Maswa
Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Maswa mkuu wa wilaya Mhe Aswege Kaminyoge amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassani kwa kuelekeza fedha hizo zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za uhuru kwenda kujenga shule 8 za watoto wenye mahitaji maalumu
Pia mkuu wa wilaya amewapongeza wadau mbalimbali kwa kufika katika kongamano hilo ili waweze kupata mwanga namna ambavyo serikali imepiga hatua toka kipindi cha Uhuru mpaka sasa miaka 61na kwenda kuwaeleza wananchi maendeleo ambayo yamefanyika tangu uhuru mpaka leo.
Wakitoa taarifa kwa wadau hao sekta mbalimbali zimeeleza mafanikio ambayo yamepatikana tangu uhuru mpaka sasa serikali imepiga hatua kubwa sana kwenye miradi ya maendeleo katika wilaya hii ya Maswa
Maji ni uhai kauli hii inakuja ikiwa nchi ya Tanzania inaadhimisha miaka 61 ya uhuru kutoka kwa wakoloni tatizo la maji limesababisha ndoa nyingi kuvunjika, watu kutembea umbali mrefu kutafuta maji lakini serikali kupitia wizara ya maji ililiona hilo na kuja na mwarobaini wa tatizo hilo kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini.
Katika wilaya ya Maswa tatizo la maji katika miaka ya arobaini lilikuwa kubwa sana na kupelekea wananchi kuhangaika sana kwa kuwa kulikuwa na kisima kimoja tu hapa mjini kilichokuwa mlima wa Nyalikungu, baadaye bwawa la Zanzui lilitengenezwa lakini halikuweza kukidhi mahitaji ya wananchi wote.
Akitoa taarifa ya mafanikio katika sekta ya maji mwakilishi wa Mkurugenzi wa MAUWASA amesema katika wilaya ya Maswa hapakuwa na Maji ya uhakika kabla ya uhuru lakini baada ya uhuru Viongozi mbalimbali walifanya juhudi kubwa ambazo zilileta matokeo na kuweza kupatikana chanzo Cha kudumu Cha bwawa la Zanzui maarufu “New Sola” ambalo linahudumia mji wote wa Maswa, mtandao wa mabomba umeongezeka na kuwa kichochea Cha maendeleo katika wilaya ya Maswa bwawa hilo linahudumia takribani wananchi wote wa Maswa mafanikio makubwa ambayo serikali imeyafanya na inaendelea kuyafanya katika mji wa Maswa na vijiji vya Maswa kwa kuwa Sasa maji yanapatikana kwa asilimia 78.4 mjini
Kwa upande wa vijijini maji yanapatikana kwa asilimia 74.5, visima vifupi 1500 vimejengwa ambavyo vinatumia pampu za mkono, visima virefu 12 ambavyo vinatumia huduma ya mtandao wa Bomba, pia serikali imefanya jitihada kubwa kwa kuweka mtambo wa kutibu na kusafisha maji katika bwawa hilo ambalo limepunguza magojwa ya mlipuko.
Aidha serikali imeendelea kuongeza miundombinu ya maji ambapo kuna mradi wa bonde la ziwa Victoria ambao utasaidia wananchi wa vijiji vya Sen'gwa, Mwabomba na maeneo mengine ya mji wa Maswa, pia miradi mingine 4 ya UVICO Sulu kwenda Inenwa mpaka Kizungu na maeneo jirani.
Hii ni sekta ambayo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa Elimu kabla ya uhuru ilitolewa ili kusaidia wakoloni katika shughuli zao lakini baada ya uhuru serikali ilikuja na azimio la Arusha ambalo lililenga kutoa Elimu ya kujitegemea na ujamaa, tangu mwaka 1961 kulikuwa na Shule 39 tu za sekondari nchi mzima
Kwa upande wa wilaya ya Maswa haikuwa na Shule ya sekondari wakati huo wa uhuru lakini serikali za awamu zote ziliweka juhudi ya kujenga shule mpaka kufikia sasa Maswa ina jumla ya Shule za Sekondari 45 zenye wanafunzi zaidi ya 7000 na vyumba vya madarasa 352 kutoka ziro mwaka 1961
Hii imechangia kwa kiasi kikubwa miradi mingi ya Elimu kukamilika na kuongeza ufaulu wa wanafunzi kwa kuwa hali ya ufaulu imefikia asilimia 97 kwa upande wa kidato Cha nne na asilimia 100 kidato cha Sita. Kwa upande wa Sekondari hayo ni mafanikio makubwa sana yaliyofanywa na serikali mpaka sasa miaka 61 ya uhuru na Shilingi bilioni 3.9 zimetolewa katika sekta ya Elimu kwa ajili uwekezaji mwaka 2021 mpaka sasa .
Maendeleo hayawezi kupatikana pasipo kuwepo kwa nishati ya umeme katika kipindi Cha miaka ya 1961 wilaya ya Maswa haikuwa na umeme lakini serikali imewekeza fedha nyingi ili kuhakikisha wananchi wa Maswa wanapata umeme na leo Tanzania inaadhimisha miaka 61 ya uhuru katika wilaya ya Maswa kwa kuwa na mafanikio makubwa.
Akiwasilisha taarifa hiyo mwakilishi wa meneja wa TANESCO wilaya ya Maswa Ndg Ali Nkuba amesema umeme ulifika Maswa mwaka 1992 na ilikuwa ni eneo la hapa mjini tu lakini maendeleo yamefanywa na serikali kwa kuwa mpaka sasa vijiji vyote 120 vya Maswa vimepata umeme na serikali inaendelea kusambaza umeme mpaka kwenye kila Kitongoji ili kumwezesha kila mwananchi aweze kunufaika na huduma hiyo ambayo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Serikali.
Pia Nkuba amewahakikishia wananchi wa Maswa kuwa tatizo la umeme litapungua kwa kiasi kikubwa kwa kuwa tayari kuna mradi mkubwa wa kujenga kituo Cha kupozea umeme kitajengwa Kijiji Cha Imalilo wilaya ya bariadi.
Huduma ya afya ilianza rasmi mwaka 1959 katika Kijiji cha Malya Magereza , Mpindo 1960 na jengo la magreth kama zahanati na baadae kuwa hospitali ya wilaya hivyo kabla ya uhuru kulikuwa na hospitali tatu.
Huduma za afya zimeendelea kuongezeka ambapo mpaka sasa kuna vituo 54 vya Serikali vinavyofanya kazi katika maeneo mbalimbali, Hospitali ya Wilaya 1, Vituo vya Afya 4 na Zahanati 49, Vituo 2 kutoka mashirika ya dini na Zahanati 2 vya Magereza ya Maswa na Malya pamoja na Zahanati 2 za watu binafsi.
Akiwasilisha taarifa hiyo katika kongamano hilo Mganga Mkuu wa Wilaya amesema huduma za afya zimefika vijiji 51 ambavyo kuna Zahanati na Vituo vya Afya na vingine vinaendelea kijengwa mpaka kufikia mwaka huu kutakuwa na zahanati na vituo vya afya 64 vinavyotoa huduma hiyo, hayo ni mafanikio makubwa ambayo serikali imeyafanya katika Wilaya ya Maswa .
Pia kwa kujengwa kwa vituo hivyo vinne vya afya ambavyo vina uwezo wa kufanya upasuaji itapunguza vifo vitokanavyo na uzazi hasahasa mama mjamzito badala ya kusafiri umbali mrefu sasa ataweza kupata huduma hiyo hukohuko kwenye kituo Cha karibu yake.
Mganga Mkuu amebainisha kuwa Hospitali imeimarisha huduma za dawa kwa kuwa dawa muhimu zote zinapatikana kwa asilimia 97 na pia majengo yameendelea kuboreshwa kwa kujenga jengo la dharura ambalo litaokoa maisha ya wanachi wengi wa Wilaya ya Maswa.
Kwa upande wao wadau mbalimbali wameipongeza serikali kwa kuendelea kuleta maendeleo katika Wilaya ya Maswa na kuomba amani na upendo iendelee kudumu, pia wameomba watendaji waendelee kukemea tabia ya ukatili wa kijinsia na kuwashirikisha wadau kwenye vikao mbalimbali nao waweze kuchangia mawazo ya kuipeleka mbele Wilaya ya Maswa katika maendeleo .
Pia wameiomba Serikali kuongeza vyuo vya VETA ambavyo vitasaidia watoto waliomaliza shule waweze kupata mafunzo ambayo yatawasaidia kujiajili wenyewe, wataalamu kusimamia kwa karibu miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ili idumu zaidi pamoja na ukarabati wa Barabara ambazo hazipitiki ikiwepo ya Malampaka mpaka Mwigumbi.
Maadhimisho hayo yamehitimishwa kwa kutoa zawadi mbalimbali kwa wanamichezo ambao walishinda katika uandishi wa insha na mpira wa miguu na kuwasisitiza wananchi wote kutangaza maendeleo yaliyofikiwa miaka 61 ya uhuru.
"Amani naupendo ndio nguzo ya maendeleo yetu"
Mgeni rasmi Mhe. Aswege Kaminyoge Mkuu wa Wilaya ya Maswa akifungua kongamano la maadhimisho ya miaka 61 ya Uhuru 9/12/2022
Wadau mbalimbali waliohudhuria kongamano la miaka 61 ya Uhuru katika Ukumbi mkubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa 9/12/2022
Mgeni rasmi akimpongeza Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nyalikungu aliyeshinda Insha kuhusu mafanikio ya miaka 61 ya Uhuru
Katibu Tawala Wilaya ya Maswa akitoa neno la Shukrani kwa wote waliohudhuria kongamano 9/12/2022
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.