Kamati ya Lishe Wilayani Maswa imefanya kikao cha robo ya kwanza ambapo Idara mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo wamewasilisha taarifa ya utekelezaji wa afua za lishe kwa mwaka huu wa fedha.
Katika kikao hicho imetolewa taarifa ya uanzishwaji wa kiwanda cha kuchakata viazi lishe ambacho uzalishaji ushaanza na bidhaa zake ziko sokoni. Kiwanda hicho kinasaga na kupaki unga wa viazi lishe. Kutokana na hili wajumbe wa kikao wamehamasishwa na kuomba kuihamasisha au kushauri jamii ya Wilayani hapa kulima Viazi lishe kwa ajili ya kuongeza kipato na chakula ili kuboresha afya za familia zao.
Wajumbe wa Kamati hii katika hatua za kuboresha lishe ya Wana Maswa wamekubaliana kwenda kutoa Elimu kwa Wafugaji na Wananchi kwa ujumla kunywa maziwa kwa ajili ya lishe, huku wakisisitiza maziwa yasichanganywe na maji ili kuepuka kuondoa ubora wake. Sambamba na hilo wameshauri kianzishwe kituo cha kupima na kukusanya maziwa ili usalama wake kwa walaji upatikane. Pia umetolewa ushauri wa kuwepo kituo cha kupima na kusindika nyama kwa ajli ya kuangalia ubora na afya za walaji.
Ili kuboresha elimu imeshauriwa Wazazi wahimizwe kuchangia chakula kwa ajili ya Watoto wao wawapo shuleni wakati wa masomo ili kuboresha Afya zao.
Kwa kuwa bidhaa nyingi zinazotengenezwa viwandani huwa zina muda wa mwisho wa matumizi, Kamati imewashauri wataalamu wa Afya na Lishe kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye maduka ili kubaini bidhaa zinazofaa kwa matumizi na zilizoisha muda wake ama hazifai kwa matumizi. Aidha kamati imeshauri elimu itolewe kwa wananchi au jamii kuhusu kukagua au kuangalia muda wa bidhaa kama umeisha ama lah pindi wanunuapo.
Mwisho wajumbe wa kamati wamekubaliana kuifikia jamii ili kutoa elimu juu ya Lishe kwani jukumu hili ni la kila mmoja. Kwa pamoja tuijenge na kuiinua Maswa kimaendeleo.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.