Kamati ya Fedha Utawala na Mipango ikiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe Paul Maige imewapongeza viongozi wanaosimamia miradi katika Wilaya ya Maswa kwa usimamizi mzuri wa mradi unaotekelezwa katika maeneo yao.
Wajumbe wa kamati hiyo wametoa pongezi hizo kwa nyakati tofauti wakati walipofanya ziara kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo, ambapo wakiwa katika Hospitali ya Wilaya wamekagua mradi wa ujenzi wa majengo mbalimbali ikiwemo jengo la mionzi, jengo la maabara, jengo la kichomea taka na jengo la wodi ya gredi katika Hospitali hiyo iliyopo katika Kata ya Sola tarehe 06 Novemba 2024.
Kwa upande wake mjumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyabubinza Mhe Emmanuel Ndalahwa amemshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika Wilaya ya Maswa ikiwemo mradi wa majengo mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya.
Pia mjumbe huyo alitaka kufahamu kama mradi huo utakamilika kwa muda uliopangwa, akijibu swali la mjumbe huyo Mganga Mkuu wa Wilaya Dr Hadija Zeggega amesema mradi huo utakamirika kwa wakati kwa kuwa mkandarasi yupo katika hatua za ukamilishaji na kuweka milango katika jengo la mionzi.
Mjumbe wa kamati hiyo Diwani wa Kata ya Jija Mhe. Walwa Lubinza amewapongeza viongozi wa Hospitali kwa kuwa kazi imefanyika kwa kiwango kikubwa katika majengo yote pamoja na kusimamia vizuri fedha za miradi.
Pia mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Diwani wa Kata ya Mbaragane Mhe. Abel Masunga amewataka viongozi hao kuendelea kuwa na moyo wa kusimamia fedha za serikali zinapotolewa ili kuhakikisha zinakamilisha mradi kwa muda muafaka.
Akisoma taarifa hiyo kwa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Maswa Dr Deogratias Mtaki amesema Wilaya ya Maswa ilipokea fedha kiasi cha shilingi milioni 900 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme katika Hospitali ya Wilaya.
Pia amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi aliyepatikana kupitia mfumo wa NEST ambapo mradi huo ulianza tarehe 14 Februari 2024 na ulitarajiwa kukamilika 12 oktoba 2024 lakini mkandarasi aliomba kuongezewa muda na sasa mradi huo atakabidhi 15 Novemba 2024.
Pia amefafanua matumizi ya fedha hizo ambapo amesema jengo la miozi litagharimu zaidi ya milioni 256, jengo la maabrara lina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 322, jengo la wodi ya gredi lina thamani ya zaidi ya shs 231 na jengo la kichomea taka lina thamani ya zaidi ya shs milioni 41.
Aidha mganga mfawidhi amesema wilaya imeendelea na ukarabati wa miundombinu ya umeme yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 47 katika majengo 6 ambayo ni wodi ya watoto, RCH, wodi ya wazazi, bima, stoo ya dawa pamoja na power house block ambapo mpaka sasa fedha zilizotumika ni shilingi milioni 408.9 na kiasi kilichobaki ni shilingi milioni 419.
Aidha Dr Mtaki amesema mradi huo utakapokamilika utasogeza huduma kwa wananchi, kuongeza wigo wa matumizi ya Teknolojia na ufungaji wa mitambo ya kisasa ya maabara na mashine ya mionzi itawapunguzia wananchi adha ya kutembea umbali wa kilometa 53 waliokuwa wanatumia kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Simiyu.
Pia wajumbe wa kamati hiyo wamekagua mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala, mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mtumishi ( 2 in 1) katika Zahanati ya Mwang’anda iliyopo Kata ya Kadoto pamoja na mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu 6 ya vyoo katika shule ya msingi Mwawayi iliyopo Kata ya Nyalikungu.
Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ikikagua ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Maswa tarehe 06 Novemba 2024
Muonekano wa Jengo jipya la Maabara katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa
Muonekano wa Jengo jipya la Wodi ya gredi katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa
Muonekano wa Jengo jipya la kichomea taka katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mwawayi akitoa maelezo kwa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango wakati ilipotembelea na kukagua ujenzi wa Vyumba vinne vya Madarasa na Matundu sita ya choo tarehe 06 Novemba 2024
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa akitoa maelezo kwa Kamati ya Fedha, Utawala na Mipango wakati ilipotembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa majengo ya Maabara, Mionzi, Wodi ya gredi na kichomea taka tarehe 06 Novemba 2024
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.