Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mh Dkt Vincent Anney leo Machi 07,2025 ameongoza kikao cha kamati ya huduma za afya ya msingi Wilaya ya Maswa ( PHC) chenye lengo la kujadili tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Marburg.
Akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya amewataka wataalamu wa afya kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi wote ili waweze kujikinga na ugonjwa huo ambao ni hatari sana kwa maisha ya mwanadamu.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dr Hadija Zegegga amesema virusi vya Marburg vinaambukizwa kwa kugusa majimaji ya mwili kama vile matapishi, damu, kinyesi jasho na mkojo, kula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa ambao ni popo, nyani, tumbili pamoja na sokwe pamoja na kugusa vitu vilivyotumiwa na mtu mwenye ugonjwa wa Marburg.
Pia ameongeza kuwa dalili za mtu mwenye ugonjwa wa virusi vya Marburg ni maumivu ya kichwa, kizunguzungu, maumivu ya misuli, kuharisha, homa, mwili kuishiwa nguvu pamoja na vidonda vya koo.
Aidha Dr Zegegga amesisitiza kuwa ili kuepukana na ugonjwa wa virusi vya Marburg wananchi wanatakiwa kujikinga kwa kuepuka kugusa majimaji ya mwili, kuepuka kula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa, kunawa kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara na kuepuka kugusa vitu vilivyotumiwa na mtu mwenye ugonjwa wa Marburg.
Mganga Mkuu amesema Wilaya ya Maswa imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inakabiliana na mlipuko huo kwa kufanya uchunguzi wa wagonjwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya kwa kuzingatia miongozo.
Kuandaaa vifaa na dawa kwa ajili ya kukabiliana na na mlipuko endapo utatokea, kutoa elimu kwa jamii ya jinsi ya kutambua dalili za ugonjwa na jinsi ya kujikinga na ugonjwa wa virusi vya Marburg pamoja na kuandaa jengo ambalo litatumika kuhudumia wagonjwa hao endapo mlipuko utatokea
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.