Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyoge ameagiza Shule zote kusaga mahindi katika mashine zenye virutubisho ili Watoto wa shule za awali, msingi na sekondari wapate vyakula vyenye virutubisho ambavyo vitawasaidia katika makuzi yao na kuwa na msingi mzuri wa elimu.
Kaminyoge ametoa agizo katika kikao cha lishe cha robo ya kwanza ya mwaka 2023/2024 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa wilaya kilichohudhiriwa na watendaji wa Kata, wakuu wa Divisheni zinazohusika na masuala ya afua za lishe pamoja na viongozi wa dini.
"Ili utengeneze jamii bora anza na msingi mahususi wa lishe mtu anaweza akaanza awali, akaenda darasa la kwanza akamaliza la saba hajui kusoma na kuandika hata ukimtandika viboko 30 kwa sababu ya kukosa lishe bora, viongozi wa dini wako hapa kutusaidia kuwaambia waumini ili ikifika miaka 20-30 ijayo kizazi hiki kiwe tofauti kinafundishika kutokana na kutumia lishe bora." Amesema Mkuu wa Wilaya
Aidha amewashukuru world vision kwa kuanzisha programu ya kutoa elimu ya lishe kwa akina mama, na watoto ambayo itakuwa kwa kipindi cha miaka saba katika Kata 25 na Vijiji 50 lengo ni kuhakikisha Watoto chini ya miaka 5 wanapata viini lishe, na akina mama kuhakikisha wanapata madini chuma.
Katika hatua nyingine Kaminyonge alisema vijana barehe wa kike na kiume kuhakikisha wanapewa elimu na viini lishe ili kuepukana na udumavu.
Mhe Kaminyoge ameongeza kuwa jukumu kubwa la watendaji wa Kata ni kuhakikisha wanasimamia Watoto wote chini ya miaka 5 na akina mama wanapata viini lishe na madini chuma ambavyo kwa pamoja vitawasaidia kuondoa udumavu kwa watoto katika maeneo yao.
"Tunaposema tumesaini mkataba wa kufuatilia na kusimamia afua za lishe ambao Mhe. Rais aliagiza yanatakiwa matokeo yaonekane matokeo ya kwenye makaratasi yawe na uhalisia, tunaposema akina mama kwenye wilaya yetu hawajifungui watoto wenye mgongo wazi iwe kweli asilimia mia moja hawajifugui watoto hao." alisema Mhe Kaminyoge.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bw. Maisha Mtipa aliwataka watendaji wa kata kufuatilia utoaji wa chakula shuleni kwa kuwa wao ndio wakurugenzi katika maeneo yao hivyo wanawajibu wa kuhakikisha wanasimamia shughuli zote zinazofanyika katika maeneo yao ikiwepo na miradi ya maendeleo.
Bw. Mtipa alisisitiza kuwa suala la lishe lisiposimamiwa vizuri katika jamii litaleta athari katika ukuaji wa watoto ambapo itapelekea changamoto katika masuala ya makuzi, kutokupata viongozi wazuri kwa sababu jamii isipopata lishe bora watoto wengi watapata udumavu.
"Suala la lishe ni ajenda kuu ambayo Mhe. Rais anaisimamia na ametoa kazi kwa wasaidizi wake ambao ni sisi tulisimamie suala la lishe tusipolisimamia vizuri tutajenga jamii ambayo sio nzuri.''alisema Mkurugenzi Mtendaji
Kwa upande wao viongozi wa dini wameishauri maeneo ya shule yote yalimwe kitaalamu kwa kuwatumia maafisa ugani kwa ajili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ili Watoto wote waweze kupata chakula shuleni ambapo itasaidia kuongeza ufaulu katika mitihani yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.