Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge amezindua rasmi msimu mpya wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2024/2025 katika Wilaya ya Maswa ambapo pamba hiyo itauzwa shilingi 1150 kwa kilo moja ya pamba ikiwa ni bei elekezi kwa mujibu wa Bodi ya pamba Tanzania na kuzitaka AMCOS zote kuhakikisha mizani zao zinakaguliwa na meneja wa vipimo wa Mkoa wa Simiyu.
“Kama kuna mzani ambao unakuja kufanya kazi katika AMCOS iliyopo katika Wilaya ya Maswa, basi huo mzani upelekwe kwa meneja wa vipimo wa Mkoa hata kama ulikaguliwa nje ya Wilaya ya Maswa kwa sababu kuna baadhi ya makampuni yametoka na mizani Singida na Shinyanga wanakuja nazo kwenye AMCOS zetu.” Mhe Kaminyoge
Pia amesisitiza kuwa mzani wowote ambao haujakaguliwa na Meneja wa vipimo wa Mkoa wa Simiyu utakuwa haujakizi vigezo hivyo hautaweza kudhibitishwa kutumika katika ununuzi wa pamba hata kama umekaguliwa sehemu nyingine.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya amesema makampuni yamekubaliana katika kikao hicho kuweka fedha katika akaunti za AMCOS wakati wa ununuzi wa pamba badala ya kuwapa fedha taslimu AMCOS kwa mkataba na AMCOS ihakikishe wananchi wakati wote wanapata pesa wanapouza pamba.
“Ili kuhakikisha tunanufaika na pamba ambayo imelimwa katika wilaya yetu, mkulima anapata kilicho chake, Halmashauri inapata kilicho chake kwa mujibu wa sheria, AMCOS na unioni inapata kilicho chake.” Mkuu wa wilaya
Pia kikao hicho kimekubaliana kuhakikisha kufuta madeni ya AMCOS kwa makampuni, kufuta madeni ya makampuni kwa AMCOS, kufuta madeni ya ushuru kwa Halmashauri ili kuodoa kero hiyo ambayo inatokea ili iishe kabisa.
Kwa upande wake Meneja wakala wa vipimo Simiyu Ndg Francis G. Olwero amewataka AMCOS kuhakikisha mizani zao zimekaguliwa hata kama mizani zao zitakuwa zimekatiwa risiti ili kuona kama inapima vizuri.
Pia amewasisitiza wanunuzi wasinunue mizani bila kufuata ushauri kwa wakala wa vipimo ili kuepuka kukamatwa.
Nae Meneja Mkuu wa SIMCU Simiyu Ndg Fares Muganda amewataka viongozi wa AMCOS kuhakikisha wanachagua viongozi ambao wana weredi ili kujenga heshima kwa AMCOS kwa sababu serikali imewapa heshima kubwa kwa kuwa sasa hakuna SIMIYU MODEL.
“Naamini kabisa Mkuu wa Wilaya kaonyesha kwa dhati jinsi anavyokerwa na hii tabia inayotokea naamini tukipata viongozi wazuri chini ya usimamizi wa mkuu wetu wa wilaya itakuwa ni historia kwa hayo yote yaliyotokea.” Ndg Muganda
Nae Mkaguzi wa pamba Wilaya ya Maswa Ndg Ally Mabruki amesema muongozo kutoka bodi ya pamba Tanzania unawataka wanunuzi wote kununua pamba kupitia vyama vya msingi yaani AMCOS zilizopo katika maeneo husika ambapo amesema pamba yoyote itakayouzwa nje ya mfumo wa vyama vya ushirika itataifishwa na serikali.
Mkuu wa Divisheni ya kilimo, mifugo na uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Robert Urassa amesema Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na bodi ya pamba poja na AMCOS imepanga jumla ya vituo 256 ikiwa ni ongezeko la vituo 2 vipya katika msimu huu hasahasa katika maeneo ya mipaka ya Wilaya jirani ili kupunguza utoroshaji wa pamba iliyozalishwa ndani ya Wilaya ya Maswa.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.