Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amezindua baraza la wafanyabiashara wa sekta ya umma na sekta binafsi kwa lengo la kujadili changamoto mbalimbali za wafanyabiashara wa Maswa zinazokwamisha katika kuendeleza biashara zao.
Mhe Kaminyoge amemshukuru Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Tanzania inakuwa na viwanda na hasa kufikia uchumi wa kati kwa kuboresha na kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini.
Amesema hayo katika uzinduzi wa baraza la wafanyabiashara wa Wilaya ya Maswa lililofanyika leo tarehe 25 Marchi 2024 na kuhudhuriwa na wakuu wa taasisi za umma, wakuu wa Divisheni husika, pamoja na wajumbe wa sekta binafsi.
“serikali kupitia Wilaya ya Maswa imehakikisha upatikanaji wa ardhi, miundombinu ya msingi huduma bora za jamii na kuimarisha jukwaa la mahusiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kupitia mabaraza ya biashara.” Mkuu wa Wilaya
Pia ameongeza kuwa baraza lina jukumu la kuhakikisha sekta ya umma na sekta binafsi zinasaidiana ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, uchumi wa familia, uchumi wa kaya, Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Amesema sekta binafsi ni muhimu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda katika Wilaya ya Maswa kwa sababu biashara ya uwekezaji inayofanyika katika Wilaya inaaksi dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na mpango wa Taifa wa miaka 5 pamoja na mikakati ya Halmashauri na taasisi zote zilizopo katika Wilaya ya Maswa.
Pia amesema baraza hilo ni chombo muhimu kwa ajili ya kukuza na kuendeleza sekta binafsi na uchumi wa Wilaya ya Maswa ambapo Baraza hilo litajadili fursa zilizopo na kutatua changamoto zilizoathiri biashara na uwekezaji.
Ameongeza kuwa hayo ni maagizo ya Mhe Rais kuhakikisha wasaidizi wake wanasikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara pamoja na kuratibu majadiliano katika ngazi ya Wilaya kwa ajili ya kutatua kero ambazo zinakwamisha wafanyabiashara katika kuendeleza biashara zao.
"Ndugu viongozi wa Wilaya ni wajibu wetu kuratibu vikao pamoja na kuhakikisha changamoto zinazoikabili sekta binafsi ya Wilaya yetu pamoja na mapendekezo yatakayowasilishwa na wafanyabiashara yanatekelezwa kwa wakati ili kuboresha Mazingira ya wafanyabiashara." Amesema Mhe Kaminyoge
Amesema adhima ya serikali ya Wilaya ya Maswa ni kuboresha Mazingira ya wafanyabiashara na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje kwa kuondoa vikwazo vya kibiashara vikiwepo kuondoa tozo zisizo na tija pamoja na kuweka miundombinu yote katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji kwa lengo la kukuza biashara na uwekezaji .
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.