Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge amewaongoza wananchi wa Maswa katika zoezi la kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa serikali za mitaa ili kupata sifa ya kuwachagua viongozi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika 27, Novemba 2024.
Mhe. Kaminyoge amejiandikisha leo tarehe 11, Oktoba 2024 katika kituo cha uandikishaji kilichopo Chuo cha Ufundi Stadi Binza njiapanda ya Lalago katika Kitongoji cha Mwantoja, Kata ya Nyalikungu Wilayani Maswa Mkoani Simiyu.
Pia Mkuu wa Wilaya amewaomba wananchi wote wenye sifa ya kuandikishwa katika Wilaya ya Maswa wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika vituo vya kupigia kujiandikishia katika vitongoji 510 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
“Niwaombe wananchi wote jitokezeni kwa wingi kujiorodhesha kwa sababu ni haki ya kikatiba ya kila raia mwenye sifa ya kujiandikisha aweze kupiga kura kwa mujibu wa sheria kwa sababu viongozi wa serikali za mtaa ndio msingi wa viongozi katika nchi yetu.” Ameeleza Mkuu wa Wilaya
Aidha amesema wananchi watakaojiandikisha ni wale wote waliofikisha miaka 18 na kuendelea, awe mtanzania na awe na akili timamu.
Pia Mkuu wa Wilaya amesisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kujiandikisha kwenye kitongoji husika ili wawe na nafasi ya kuwachagua viongozi wao wa serikali za mitaa katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024 ambapo watawachagua Mwenyekiti wa kitongoji husika, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji, wajumbe wa serikali ya kijiji na wajumbe wa viti maalumu wa serikali za vijiji.
“Mjitokeze kwa wingi kujiandikisha ili mchague viongozi ambao ni wachapakazi wenye uwezo wa kuwongoza wananchi kwenye shughuli za maendeleo na mambo mbalimbali katika maeneo yao.” Amesema Mhe Kaminyoge
Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi Halmashauri Wilaya ya Maswa Ndg. Maisha Mtipa amesema katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Kuna watu zaidi ya laki nne lakini katika zoezi hilo wanatarajia kuandikisha Zaidi ya wananchi laki mbili katika daftari la wapiga kura ambalo limeanza leo terehe 11- 20 Oktoba 2024 na kuhitimishwa tarehe 20.10.2024.
Pia Ndg. Mtipa amesema vituo hivyo vinapatikana katika Kila kitongoji ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ina vitongoji 510 ambapo vitongoji 40 vipo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Maswa.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wote kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari la wapiga kura ili wakati wa Uchaguzi wasikose sifa ya kuchagua viongozi wanaowataka wakati wa kupigia kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika27, Novemba 2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.