Mkuu wa wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu Mhe. Aswege Kaminyoge ameishukuru Mahakama na vyombo vingine vya kutoa haki jinai kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutoa elimu na haki kwa kuzingatia misingi ya haki ili wananchi wapate haki stahiki.
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo katika kilele cha wiki ya sheria iliyofanyika katika viwanja vya mahakama yenye kauli mbiu ya “ Nafasi ya Mahakama, wadau umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa taifa, nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai”.
Mhe. Kaminyoge amesema elimu inatakiwa kutolewa zaidi kwa wananchi ili wasitumie pesa nyingi kwa ajili ya manufaa ya familia zao kwa makanjanja ambao hawana kesi wanazunguka kuanzia asubuhi mpaka Mahakama inapofungwa kudaka watu kwa ajili ya kuwarubuni vitu mbalimbali kwenda kwa mahakimu.
Tukiweza kufanya hivyo wananchi wetu watakuwa na furaha kubwa katika nchi yao.
“Leo hii tuna viongozi wa Dini, wananchi mbalimbali, watumishi mbalimbali wana wajibu wa kuhakikisha mahali walipo wanatoa maamuzi yenye haki kwani vitabu vya Dini; Biblia na Msahafu vinazungumzia juu ya utoaji wa haki.” amesema Mhe Kaminyoge
Aidha Mhe. Mkuu wa Wilaya amesema viongozi wamepewa mamlaka na Mhe. Rais na wananchi kwa ajili kutoa haki ambapo kila mtu ajitafakali anapotoa haki ajiulize je? Ametenda haki au hajatenda haki? hivyo amewataka watumishi na mahakimu kutoa haki ili mwananchi akitoka Ofisini au Mahakamani apite kifua mbele akisema haki imetendeka.
“Niwaombe waheshimiwa Mahakimu, Wapelelezi, Wachunguzi, TAKUKURU, Magereza Wananchi wanawategemea sana; Mahakimu Mahakama zinawategemea sana kwa ajili ya kutoa haki tufanye kazi kwa kuzingatia misingi ya haki.” Amesema Mkuu wa Wilaya
Pia amemshukuru Mhe. Hakimu kwa kazi kubwa aliyoifanya katika wiki ya sheria ambapo wananchi wengi wamepata elimu ambayo itawasaidia kupata haki iliyo sahihi hivyo ameitaka Mahakama isichoke kutoa elimu kwa wananchi.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa Mhe. Enos Misana amesema maadhimisho ya wiki ya sheria yamehusisha utekelezji wa shughuli mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kwa umma kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria, upokeaji wa shida, malalamiko, maoni, mapendekezo mbalimbali kuhusiana na huduma zitolewazo na Mahakama.
Ameongeza kuwa zoezi la utoaji elimu kwa umma lilitekelezwa katika viwanja vya Mahakama ya Wilaya ambapo wananchi na wadau waliweza kujitokeza kupata elimu ya masuala ya kisheria, kuwasilisha malalamiko pamoja na kufungua mashauri kwa njia ya mtandao.
Aidha Hakimu Mfawidhi amesema malalamiko mengi yaliyotolewa yanaeegemea zaidi upande wa ardhi, ndoa, mirathi na utelekezwaji wa watoto ambapo elimu hiyo imetolewa maeneo mbalimbali ikiwepo Shule za Sekondari na maeneo ya minadani.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.