Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amegawa sare kwa Maafisa Ugani 39 wa Wilaya ya Maswa tarehe 20 Agosti 2024 eneo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetoa sare hizo kwa lengo la kuwawezesha maafisa ugani hao kufanya kazi kwa ufanisi katika maeneo yao ya kiutendaji ili kuongeza tija katika uzalishaji.
Mkuu wa Wilaya amewataka maafisa ugani wote kuhakikisha wanawafikia wakulima ili kuwapa utaalamu kwa kuwa tayari wana vitendea kazi ambavyo vitasaidia kutoa utaalamu kwa wakulima.
"Rai yangu kwenu ni kuhakikisha mnachukua nafasi hii kumzawadia Mhe Rais, kumheshimisha Mhe Rais katika hivi vitendea kazi alivyovigawa, matokeo ya uzalishaji katika msimu ujao yaongezeke maradufu kama sio mara tano kwa sababu hatuna nafasi ya kusingizia pikipiki wote 39 mnazo, vitendea kazi vingine mnavyo. Hakuna sababu nyingine ya Afisa yeyote, mtaalamu au kiongozi yeyote akipita kwenye maeneo yenu ya kazi akute mazao yapo chini ya kiwango." Amesema Mhe. Kaminyoge
Ameongeza kuwa Maafisa Ugani hao wanatakiwa kutoa Elimu kwa wananchi kuhusu kanuni bora za Kilimo ili uzalishaji wa mazao uwe na tija ambapo katika zao la pamba uzalishaji utoke kwenye kilo 250 hekari moja mpaka uzalishaji ufikie kilo 1000 hadi kilo 2500 kwa hekari moja.
Aidha Mkuu wa Wilaya amemshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazozifanya katika kukuza na kuimarisha sekta ya kilimo.
Pia ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya kwa namna alivyojipanga ili kuhakikisha Wilaya ya Maswa inazalisha mazao mbalimbali kwa tija yakiwemo mazao ya kimkakati kama zao la pamba, alizeti na mazao mengine.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya amewataka Maafisa Ugani hao kuanzisha vipando vya mazao mbalimbali ili wananchi waweze kujifunza namna bora ya kilimo ambacho kitaleta tija.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Ndg. Maisha Mtipa amesema Wizara ya Kilimo imejipanga kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya Kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ambapo Wizara ya Kilimo imejikita kuleta vifaa ili kuweza kuboresha uzalishaji.
Pia Ndg. Mtipa amewataka Maafisa Ugani kilimo kuhakikisha wanavaa sare hizo wakati wakitekeleza majukumu yao kwa wananchi na katika maeneo yao ya kazi.
Hapa chini ni picha mbalimbali wakati Mhe Mkuu wa Wilaya akikabidhi Sare kwa Wagani Kilimo
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.