Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge ameipongeza Halmshauri ya Wilaya ya Maswa kwa kutenga bajeti ya shilingi milioni 70 kwa ajili ya kuanzisha kitalu cha miche mbalimbali ambayo itapandwa katika taasisi mbalimbali za serikali na watu binafsi ili kurudisha uoto wa asili na kuhifadhi mazingira.
Mhe. Kaminyoge Alitoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika wilaya ya maswa kwa mwaka 2023/2024 ambalo lilifanyika katika Shule ya Sekondari Zanzui iliyopo Kata ya Zanzui, ambapo zaidi ya miti 600 ilipandwa katika eneo la shule hiyo.
Pia ameongeza kuwa katika Wilaya ya Maswa kuna tatizo la ukame kutokana na uharibifu wa mazingira ambao unatokana na ukataji wa miti hivyo amewata viongozi pamoja na wananchi kuwa jukumu kubwa lililopo ni kuhakikisha uoto wa asili unarudi katika Wilaya ya Maswa.
“Msingi mkubwa wa utunzaji wa mazingira ni kuhakikisha tunapanda miti, miti tukiipanda ndio itakayoturejeshea hali nzuri ya tabianchi Mhe. Rais ametuagiza viongozi wote katika ngazi mbalimbali kuanzia Kitongoji, Kijiji, Kata na Wilaya kwa ujumla wake kuhakikisha kila msimu wa mvua unapoanza tupande miti milioni moja na laki tano kwa mwaka.”alisema kaminyoge
Mkuu wa Wilaya ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji na wananchi kuhakikisha miti inapandwa kama alivyoelekeza Mhe. Rais hivyo amezitaka taasisi zote kupanda miti ambayo itasaidia wananchi kujifunza kwa vitendo kutokana na miti ambayo watakuwa wameipanda.
Pia Mhe. Kaminyoge alizitaka taasisi zote za shule kuandaa vitalu vya miche 20000 kila shule ili kufikia lengo la Mhe Rais la kupanda miche milioni moja na laki tano kila mwaka kwa kuisaidia Halmashauri kujitosheleza ili isitafuta miti kwenye makampuni mengine.
Awali akitoa taarifa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bw. Maisha Mtipa alisema wametengeneza kitalu chenye jumla ya miti 421000 ambayo itagawiwa katika taasisi mbalimbali za halmashauri ikiwepo vituo vya Afya, Shule za msingi na sekondari pamoja na Zahanati ili kutunza mazingira.
“Kwa kufanya hivi tunaendeleza sera ya serikali ya utunzaji wa mazingira katika nchi yetu na tukiangalia katika maeneo yetu ya Wilaya ya Maswa maeneo mengi hayana miti, sisi Halmashauri tunafanya juhudi kubwa ya kupanda miti ili tulejeshe uoto wa asili wa eneo la Maswa.” Alisema Mkurugenzi Mtendaji
Nae wakala wa Misitu Wilaya ya Maswa (TFS) Bw. Fabian Mosha alisema kutokana na changamoto ya ukame iliyopo Maswa, Wilaya imejidhatiti kupanda miti milioni moja na laki tano ili kuhakikisha kuwa agizo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan linafikiwa katika msimu huu wa mvua wa mwaka 2023/2024.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zanzui Bw. Juma Selemani alimshukuru Mhe Dkt Samia Suhulu Hassan kwa kuhamasisha nchi kurudisha uoto wa asili kwa kupanda miti hivyo mwenyekiti huyo ameahidi kusimamia miti yote iliyopandwa katika eneo hilo na alisema wataendelea na zoezi hilo la kupanda miti katika Kijiji hicho.
Kwa upande wake mwanafunzi wa shule ya Sekondari Zanzui Maria Maduhu anayesoma kidato cha tatu wameahidi kuitunza miti hiyo ambayo itawaletea faida mbalimbali zikiwepo kupata hewa safi sambamba na kuzuia mmomonyoko wa ardhi.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.