Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge amewaagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya, Afisa ushirika na makampuni kuandaa mikataba madhubuti yenye mashiko ya kisheria ambayo itasainiwa na pande mbili baina ya makampuni na makatibu wa AMCOS wakati wa zoezi la ununuzi wa pamba ili kuepusha upotevu wa Fedha na madeni.
Pia Mkuu wa Wilaya amesema mikataba hiyo ikikiukwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwepo kupelekwa mahakamani ambapo yeyote atakayekiuka atakuwa ameshitakiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sio kampuni.
Ametoa maagizo hayo katika kikao cha wadau wa pamba kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa tarehe 20 Mei 2024.
Mhe Kaminyoge pia ameyataka makampuni hayo kutoa taarifa katika ofisi yake kabla ya makabidhiano ya mikataba na AMCOS ili kupunguza mlundikano wa Fedha za makampuni mengi kwa AMCOS moja ambayo haitakuwa na uwezo wa kutoa pamba hiyo.
Aidha ametoa wito kwa makampuni yote kuhakikisha yanapokabidhi Fedha hizo kwa makatibu wa AMCOS lazima wawepo wajumbe wengine wa Bodi ya pamba sambamba na hilo amewataka makatibu wa AMCOS, makarani na wahasibu mikataba yao iwe na uhai ili kutekeleza yale yote yanayotokea kama matatizo na migogoro wakati wa ununuzi wa pamba.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya amezitaka AMCOS zote ziwe na mashine ya kuhesabia Fedha kwa ajili ya kuhakiki ili kuepusha upotevu wa Fedha ambao unatokea wakati wa makabidhiano bila kuhesabu ambao unasababisha AMCOS kuwa na madeni makubwa.
"Afisa ushirika wewe ndio Mkaguzi wa hapa wilayani hakikisha Kila AMCOS inakuwa na mashine za kuhesabia pesa na hao waliochaguliwa juzi uwafundishe namna ya kutumia hizo pesa." Mkuu wa Wilaya
Aidha Mkuu wa Wilaya amezitaka AMCOS kuwa na ubunifu wa kukopa benki ili wawe na uwezo wa kujiendesha wenyewe kwa kufanya biashara na makampuni wakati wa kununua pamba makampuni yawe yananunua pamba kwao na sio kwa mkulima.
Kwa upande wake Mrajisi wa Vyama vya ushirika Mkoa wa Simiyu Ndg. Godfrey Mpepo ameyataka makampuni yote yanayonunua pamba kabla hayajapeleka Fedha kwa AMCOS yatoe taarifa kwa mkuu wa Wilaya kuhusu kiwango Cha Fedha na mzigo wanaouhitaji ili kuepusha mlundikano wa Fedha katika AMCOS moja kwa sababu ya uchache wa pamba.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.