Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mhe Paul Maige amezindua kampeni ya chanjo ya homa ya mapafu kwa ng'ombe katika wilaya ya Maswa ili kuhakikisha Mifugo inakuwa na afya Bora yenye kuleta matokeo chanya kwa wafugaji na kukidhi vigezo vya kitaalamu katika udhibiti wa magonjwa .
Amesema hayo katika uzinduzi wa chanjo hiyo katika kijiji cha Mwanhegele kilichopo kata ya Nyabubinza wakati akimwakilisha Mkuu Wa Wilaya ya Maswa Mhe Aswege Kaminyoge.
Mhe Mwenyekiti amesema serikali kupitia Ilani ya uchaguzi itaendelea kuboresha mifugo kwa kuwa mifugo ikiboreshwa masoko yatapatikana kwa sababu hakuna mwananchi ambaye atataka nyama ambayo haina kiwango.
“Unapojitokeza kuchanja mifugo ambayo unaifuga, unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa katika mtandao wa kupata soko la uhakika kwa hivyo wafugaji niwape rai muwe mabalozi kwa wengine ili kuhakikisha mifugo yao wanaichanja” Mhe Maige
Aidha ameongeza kuwa athari ya kutokuchanjwa kwa mifugo hiyo kwa ubora haitafanikisha malengo ya Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025.
Mhe Maige amesisistiza kuwa Mifugo ikipatiwa chanjo, malisho mazuri na maji ya uhakika, mifugo hiyo itakuwa mizuri na kuwa chachu kwa wanunuzi kununua nyama hizo kwa ajili ya matumizi ya nyama kwani itakuwa imekidhi vigezo vyote.
“Naamini ya kwamba chanjo hii ya leo tunayoshiriki tunaiunga mkono serikali kupitia Ilani ya uchaguzi ambayo ilieleza kwamba kwa kipindi cha miaka mitano tutahakikisha kwamba mifugo imeboreshwa na ikiboreshwa mfugaji atapata tija, pia chama cha wafugaji na serikali wameendelea kuchukua hatua kwa kuzielekeza taasisi za kifedha kutoa mikopo kwa wafugaji ili iwepo tija” amesema Mwenyekiti wa Halmashauri
Kwa upande wake Daktari wa Mifugo Wilaya ya Maswa Ndg Charles Msira amesema serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kutekeleza mazoezi mbalimbali ya udhibiti wa magonjwa kwa njia ya chanjo lengo ni kumuinua mfugaji kiuchumi
Daktari Msira ameongeza kuwa udhibiti wa magojwa ya mifugo unatekelezwa kwa kuzingatia sheria ya magojwa ya wanyama namba 17 ya mwaka 2003, kanuni ya chanjo na utoaji wa chanjo ya mwaka 2020 pamoja na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.
Aidha kulingana na takwimu za ng'ombe waliopigwa chapa 2017 Wilaya Ya Maswa ina jumla ya ng'ombe 305,640 ambapo lengo la wilaya ni kuchanja ngombe hao kwa asilimia 80 dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu kwa mwaka 2024 ili kukidhi vigezo vya kitaalamu katika udhibiti wa magonjwa na kwa mujibu wa kanuni ya chanjo na uchanjaji mifugo ya 2020.
Pia ametoa wito kwa mfugaji yeyote atakayekaidi kupeleka ng'ombe wake kwenye vituo vya chanjo vilivyopangwa hatua kali zitachukuliwa ambapo mfugaji atatozwa shilingi 5000 kwa kila ng'ombe kwa kuwa ugonjwa huo unaenea kwa kasi na kusababisha maambukizi makubwa ambayo yanapelekea vifo vingi vya mifugo na kuatarisha kufungwa kwa minada hivyo kupunguza pato la Halmashauri na taifa
Nae Diwani wa Kata ya Nyabubinza Mhe. Emmanuel Ndalahwa amewataka wafugaji kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo muhimu la mifugo kupata chanjo kwa kuwa masoko mengi ya nje yanahitaji uthibitisho wa chanjo na huduma zingine zilizotolewa kwa kuwa kazi ya ufugaji ni biashara kama zilivyo biashara zingine.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.