Balozi wa pPamba Tanzania Mhe. Agrey Mwanri ametoa elimu juu ya kanuni Bora za kilimo cha zao la Pamba kwa viongozi, wataalamu wananchi na watendaji kwa kuwaomba watendaji kuanzia kitongoji mpaka wilaya kuwa na mikakati mizuri na mbinu kwa kufanya wenyewe sio kutumia mwakilishi kwa kuwa kazi hiyo haitakuwa na ufanisi katika utekelezaji wake.
Akitoa elimu hiyo Balozi wa Pamba amesema kuwa elimu hiyo itasaidia wakulima namna bora ya kulima Pamba kwa kufuata taratibu zote za utayarishaji wa mashamba kwa kukata maotea yote, upandaji wa mbegu za pamba kwa kuzingatia kanuni, kutokuchanganya Pamba na mazao mengine, kupalilia palizi baada ya siku 21 baada ya Pamba kuota na kupulizia dawa kwa kufuata kanuni nzuri za unyunyuziaji ili kupata Pamba nyingi ambayo italeta manufaa.
Mhe. Mwanri amesema mpango wa taifa ni kupata Tani milioni 1 na Mkoa wa Simiyu unatakiwa kuzalisha Tani 500,000 ambazo zitagawanywa katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ambapo Wilaya ya Maswa inatakiwa kuzalisha Tani 130,000 za Pamba kwa kuwa zao hilo limechangia katika mabadiliko ya sayansi na technologia ya kisasa, ajira kwa vijana na mapato ya serikali.
Nae mkuu wa wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amesema zao la Pamba ndio kipaumbele kwa kuwa zao ambalo mkulima anapata kipato cha haraka na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia, kaya na wilaya kwa kuwa zao hilo linachangia asilimia 75 ya mapato ya Halmashauri yanatokana na ushuru wa zao la Pamba.
"Nichukue nafasi hii tena kukushukuru Balozi wa Pamba ulifanya kazi kubwa mwaka jana kazi ambayo wakulima wanaipongeza mpaka leo na kwa mara ya kwanza mimi kama Mkuu wa Wilaya wakati natembea kukagua maandalizi ya kilimo cha Pamba mwaka jana asilimia 70 ya wakulima wetu walikuwa wanapanda kwa mstari" amesema Mkuu wa Wilaya.
Mhe. Kaminyoge amewasisitiza wataalamu, viongozi na watendaji wakatoe elimu hiyo vizuri kwa wananchi kwa kuwa wananchi ni wasikivu ikiwa viongozi watakuwa wawazi kutoa elimu hiyo ambayo itawawezesha wananchi kutambua kanuni Bora za kilimo cha Pamba.
Robert Urassa Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi amesema kwa msimu huu wa kilimo Wilaya imeweka malengo ya kulima heckta 82,212 lakini mbegu zilizofika zinaweza kulima hecta 122,000 tani 2,459 ukiongeza za kilimo hai ambazo ni Tani 600, aidha wameishukuru bodi ya Pamba na Serikali kwa kuleta mbegu za kutosha maeneo mengi japokuwa kulikuwa na upungufu lakini bodi imeendelea kuleta mbegu na tayari Tani 70 zimeongezwa ili kupunguza changamoto kwa wakulima na amewaomba watendaji na viongozi kusimamia kwa karibu ili wakulima wetu walime kisasa kufikia lengo la Tani 130,000.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa amesema dhamana waliopewa viongozi ni kuwa na usimamizi madhubuti wa mamlaka za serikali za Mitaa ili kuwe na ufanisi ambao utawezesha huduma ziwe bora kwa wananchi na mapato yatakayopatikana yataboresha maeneo ya kazi na kuwa na tija ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa.
Balozi wa Pamba Tanzania atakuwa Maswa kwa ziara ya siku 7 kutembelea Kata 14 za Wilaya ya Maswa ili kutoa elimu ya kilimo bora na kanuni za ulimaji mzuri wa Pamba ambao utaleta tija katika dhahabu nyeupe zinazopatikana hapa Maswa.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.