Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini RUWASA imetenga bajeti ya shs bilioni 3.7 katika mwaka wa 2024/2025 kupitia PforR -IV kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali katika vijiji vya Wilaya ya Maswa.
Miradi ambayo itatekelezwa kupitia Fedha hizo ni pamoja na kuongeza huduma za maji kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi wa Ipililo, kuanza ujenzi wa miradi ya Budekwa- Kiloleli, kufanya utafiti Mwabayanda , kutumia chanzo Cha maji Cha Ngongwa kuongeza maji mradi wa Isulilo
Kuboresha upatikanaji wa maji mradi wa Sulu kwa kuchimba kisima Mbaragane, kuongeza mradi kwenda Kijiji Cha Manawa ili wananchi wa Kijiji hicho wapate maji ya ziwa Victoria na kuanza ujenzi wa mradi wa Funika.
Akifungua mkutano wa wadau wa sekta ya maji katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Mkuu wa Wilaya ya Maswa Mhe. Aswege Kaminyoge amesema huduma ya maji katika Wilaya ya Maswa inapatikana kwa kiwango kikubwa kwa sababu serikali imetenga Fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maji.
Ameongeza kuwa shs milioni 200 imetengwa katika vijiji vyote ambavyo havina maji vya Budekwa, Mwabaraturu, Mwamashindike , Mpindo na vingine ambavyo vina matatizo ya maji kwa ajili ya kufanya utafiti wa maji ya chini ili wananchi hao wapate maji .
"Baada ya miaka 5 au 4 ijayo Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Maswa itakuwa inapata maji kama huduma ya maji kwa asilimia 100 kwa wananchi wake kwa hiyo ni kazi yetu sisi sote kwa upande wa serikali, viongozi Waheshimiwa Madiwani na viongozi mbalimbali kuwaeleza wananchi kazi kubwa inayofanywa na serikali."
Pia ametoa rai kwa wakuu wote wa taasisi, Mkurugenzi Mtendaji, Wakuu wa idara na sekta watengeneze taarifa ambazo watawakabidhi Waheshimiwa Madiwani ili wakaeleze kwa wananchi mambo yaliyotekelezwa na serikali katika Wilaya ya Maswa.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Wilaya ya Maswa Mhandisi Lucas Maduhu amesema RUWASA inaendelea kuboresha huduma ya maji ambapo katika kipindi Cha julai 2019 hadi may 2024 RUWASA imetekeleza miradi mbalimbali yenye thamani ya shs bilioni 9.5 kupitia programu mbalimbali lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata maji Safi na salama.
Aidha katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kupitia PforR -IV RUWASA ilitengewa jumla ya shs bilioni 4.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji katika vijiji vya Wilaya ya Maswa ambapo miradi hiyo ipo katika hatua za utekelezaji.
Jukumu kubwa la RUWASA ni kusanifu miradi, kujenga miradi na kusimamia utoaji wa maji kupitia vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSOs) na ili CBWSOs ziweze kujiendesha ni lazima visima vyote vilivyopo vijijini visimamiwe na CBWSOs ili zipate pesa kwa ajili ya matengenezo.
Halmashauri ya Wilaya ya Maswa
Sanduku la Posta: 170, MASWA
simu ya Mkononi: +255 282 750 271
Simu: +255 282 750 271
Barua Pepe: ded@maswadc.go.tz
Copyright ©2022 Maswa District Council. All rights reserved.